Marsabit:
Naibu Gavana wa Kaunti ya Marsabit, Solomon Gubo, amewataka washikadau wote wanaohusika na usimamizi wa majanga kuwasilisha taarifa sahihi na za kina kuhusu athari za mvua zilizopita ili kuwezesha serikali kupanga hatua stahiki za kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.
Gubo alitoa wito huo wakati Kamati ya Kutathmini Majanga ya Kaunti (County Steering Group - CSG) ikiendelea kukusanya taarifa kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti kuhusu uharibifu uliosababishwa na mvua, hususan katika miundombinu, makazi na sekta ya kilimo.
Akizungumza na wanahabari baada ya kikao cha kamati hiyo, Gubo alisema kuwa jukumu kuu la CSG ni kufanya tathmini ya kina ya athari zilizotokana na mvua ili kubaini maeneo yaliyoathirika zaidi na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia serikali ya kaunti pamoja na serikali ya kitaifa kupanga hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo.
Book this slotAlisisitiza kuwa taarifa zitakazowasilishwa na wadau mbalimbali zinapaswa kuwa sahihi na zenye kuakisi hali halisi mashinani, akisema kuwa ubora wa ripoti hiyo utachangia kufanya maamuzi yanayolenga kuokoa maisha, kulinda mali na kupunguza madhara ya majanga katika siku zijazo.
Gubo aliongeza kuwa tathmini hiyo pia itasaidia kaunti kujiandaa vyema kwa msimu ujao wa mvua unaotarajiwa, kwa kuhakikisha maeneo yenye hatari yanatambuliwa mapema na mikakati ya kupunguza madhara inawekwa kabla ya mvua kuanza kunyesha.
Aidha, Gubo alisema Serikali ya Kaunti ya Marsabit tayari imetenga fedha za dharura zitakazotumika katika kukabiliana na athari za majanga. Hata hivyo, alieleza kuwa juhudi za serikali pekee hazitoshi na hivyo akatoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, washirika wa maendeleo pamoja na taasisi nyingine kushirikiana na serikali ili kuimarisha maandalizi na utoaji wa misaada kwa jamii zilizoathirika.
Katika suala la usalama wa chakula, Gubo alisema kuwa licha ya baadhi ya wakulima kufanikiwa kupata mavuno kutokana na mvua zilizopita, kiwango cha chakula kilichozalishwa bado hakijatosheleza mahitaji ya wakazi wengi wa Marsabit. Alibainisha kuwa baadhi ya maeneo bado yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa chakula kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na uzalishaji mdogo wa mazao.
Book this slotKutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuweka mikakati ya mapema ya kuimarisha usalama wa chakula, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi chakula na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo.
Ripoti ya tathmini ya athari za mvua, inayoratibiwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame (NDMA) kwa kushirikiana na Kamati ya Kutathmini Majanga ya Kaunti, inatarajiwa kutoa picha kamili ya kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mvua katika sekta mbalimbali. Baada ya kukamilika, ripoti hiyo itawasilishwa kwa serikali ya kitaifa ili kusaidia kupanga hatua za haraka za dharura, ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa na kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na majanga yajayo.
Comments
No approved comments yet. Be the first to join the conversation.